MAKALA YA MALOTO: Kuhamia Dodoma kumbukumbu halisi kumuenzi Mwalimu Nyerere

Hatimaye Serikali imehamia Dodoma. Uamuzi wa Rais John Magufuli kuhamia Dodoma limekamilisha safu nzima. Alianza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, mawaziri wakafuata, kisha Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na JPM.

Kama kuna mambo ambayo kwayo Rais Magufuli ametimiza ndoto ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere mojawapo ni hili la kuhamia Dodoma.

Historia inaonyesha kuwa mwaka 1967, Serikali iliipa kazi kampuni ya upangaji miji ya Canada ili kuupangilia mji wa Dar es Salaam kama makao makuu ya nchi. Kampuni hiyo ikaonyesha Dar haikufaa kuwa mji mkuu.

Ni hapo mawazo ya kuhamisha makao makuu kwenda katikati ya nchi yalianza na Dodoma ikapendekezwa na mchakato ukaanza.

Mwaka 1973, Mwalimu Nyerere aliitangaza Dodoma kuwa mji mkuu. Halafu aliyekuwa Waziri Mkuu, Rashid Kawawa alihamia huko. Alisafiri kwa treni kama hatua ya mwanzo ya Serikali kuhamia Dodoma.

Wakati Kawawa akiagwa Stesheni ya Dar es Salaam, hakuna aliyedhani kama Nyerere angemaliza miaka 12 hadi kung’atuka mwaka 1985 bila kuhamia Dodoma.

Mawaziri wakuu waliofuata baada ya Kawawa, waliishi Dodoma. Edward Sokoine, Cleopa Msuya, Salim Ahmed Salim na Joseph Warioba. Mwaka 1991, nchi ikiongozwa na Rais Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu, John Malecela alirejesha makazi ya waziri mkuu Dar es Salaam.

Wakati anafunga Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma, Malecela alitoa sababu mbili. alisema yeye kama kiongozi wa mawaziri alipata shida kuwaongoza mawaziri ambao wote waliishi Dar es Salaam.

Sababu ya pili, alisema yeye alikuwa mshauri wa Rais ambaye aliishi Dar es Salaam. Hivyo alilazimika kutumia simu au kusafiri kwenda mara kwa mara kukutana na Rais Mwinyi.

Wakati huo Mwinyi alikuwa anatokea Zanzibar na Malecela pamoja na uwaziri mkuu, alikuwa makamu wa kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Tangu nchi ilipopata uhuru 1961 hadi 1985, nchi ilikuwa changa, kulikuwa na changamoto nyingi na zilikuwa nyakati za kuunganisha jamii za makabila kuwa Taifa. Gharama za kujenga makao makuu mapya zilikuwa mzigo kwa nchi.

Mwaka 1977 nchi ikaingia kwenye msukosuko wa kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Taifa likaingia gharama za ununuzi wa ndege rasilimali nyingine ili kuanzisha mashirika ambayo awali yalikuwa chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mwaka 1978, nchi ikaingia kwenye Vita Kagera, maumivu yake ni ya kihistoria. Hivyo mazingira ya kuhamia Dodoma yalikuwa magumu.

India wakati inatawaliwa na Uingereza, mwaka 1911, Mfalme George V, alitangaza kuhamisha makao makuu kutoka Calcutta (Kolkata) kwenda New Delhi. Mpango wa kuhama ulikamilika mwaka 1931.

Kama India chini ya Uingereza ilichukua miaka 20, unaweza kujionea ilikuwa vigumu kiasi gani kwa Nyerere kufanikisha malengo yake ndani ya miaka 12 katika nchi changa.

Ipo hoja kwamba wazo la Dodoma lilitangulia kabla ya lile la kuhamisha makao makuu ya Nigeria, kutoka Lagos kwenda Abuja ambalo lilikamilishwa kwa miaka 11 tangu 1980 hadi 1991.

Hata hivyo, mazingira yaliibeba mno Nigeria. Wanigeria mbali na kupinduana kijeshi, hawawahi kupigana vita.

Mwaka 1978, Nyerere alianzisha Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) na kuipa majukumu ya kuijenga Dodoma, hatua inayodhihirisha alikusudia kuhamia Dodoma.

Mwaka 1991, wakati Serikali ya Nigeria inahamia Abuja, Rais Mwinyi alimruhusu Malecela kurejea Dar es Salaam. Japo Malecela alitoa sababu za msingi, hatua hiyo ilirudisha nyuma dhamira ya kuhamia Dodoma.

Rais Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete, wana sifa kubwa ya kujenga na kuimarisha uchumi wa nchi. Unaweza kuwatafsiri kuwa waliona nchi ikiwa na uchumi mzuri, mpango wa kuhamia Dodoma ungekamilika.

Haikuwezekana kuandika historia wakati wa Nyerere, imewezekana kipindi cha Magufuli. Mwinyi, Mkapa na Kikwete, wanastahili pongezi kwa kurahisisha mazingira, hasa kiuchumi.